´Aqiydah Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah
Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn


Utangulizi

Himdi zote anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu. Mwisho mwema ni wa wachaji Allaah na uadui ni kwa madhalimu. Ninashuhudia ya kwamba hakuna mungu mwenye haki ya kuabudiwa isipokuwa Allaah, hali ya kuwa peke yake hana mshirika, Yeye ndiye Mfalme na haki iliyo wazi, na ninashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wake, ambaye ndiye Mtume wa mwisho na kiongozi wa wachaji Allaah. Swalah na salaam zimwendee yeye, ahli zake, Maswahabah zake na wale wenye kuwafuata kwa wema mpaka siku ya
Qiyaamah.

Amma ba´d:

Hakika Allaah (Ta´ala) amemtuma Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa uongofu na dini ya haki ili awe ni rahmah kwa walimwengu, kiigiezo kwa watendaji na hoja kwa viumbe wote.

Kupitia kwake na Kitabu na Hekima Aliyoteremsha amebainisha kila kilicho na manufaaa kwa waja na kutengemaa kwa hali zao katika dini na dunia yao.

Miongoni mwa hayo ni I´tiqaad sahihi, matendo yaliyosalama, tabia nzuri na adabu iliyo juu. Akauacha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Ummah wake katika njia ilio wazi kabisa; usiku wake ni kama mchana wake na hakuna mwenye kuiacha isipokuwa mwangamivu.

Njia hii ikafuatwa na Ummah wake ambao umemuitikia Allaah na Mtume Wake.

Wao, Maswahabah, Taabi´uun na wale waliowafuata kwa wema ndio viumbe bora. Wakasimamisha Shari´ah yake, wakashikamana na Sunnah zake na wakaziuma kwa magego yao katika ´Aqiydah, ´ibaadah, tabia na adabu. Wao ndio walikuwa wale watu ambao daima ni wenye kushinda na wako wazi wazi juu haki. Hawawadhuru wale wenye kuwapinga na kwenda kinyume nao mpaka ije amri ya Allaah (Ta´ala) ilihali bado wako katika hali hiyo.

Sisi tunafuata nyayo zao na kwa msaada wa njia yao yenye kusapotiwa na Kitabu na Sunnah tumeongoka - tunamshukuru Allaah kwa hilo. Tunasema haya kwa kutaja neema ya Allaah (Ta´ala) aliyotutunukia na kubainisha yale ambayo ni wajibu kwa kila muumini kuwa juu yake.

Tunamuomba Allaah atuthibitishe sisi na ndugu zetu waislamu kwa kauli thabiti duniani na Aakhirah na atutunukie rahmah Zake - hakika Yeye ndiye mwingi wa Kutunuku.

Kutokana na umuhimu wa maudhui hii na kutofautiana kwa matamanio ya watu, nimependa kuandika kwa mukhtasari ´Aqiydah yetu, ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Imani hiyo ni kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Wake, siku ya Mwisho na Qadar; kheri na shari yake. Ninamuomba Allaah (Ta´ala) ajaalie iwe Khaalisw kwa ajili ya Uso Wake, yenye kuafikiana na radhi Zake na yenye kuwanufaisha waja Wake.