Sujuud, kuinuka kutoka katika Sujuud na yenye kuhusiana nayo

Sujuud, kuinuka kutoka katika Sujuud na yenye kuhusiana nayo

9- Asujudu na wakati huo huo aseme "Allaahu Akbar" na huku atangulize magoti kabla ya mikono yake - iwapo kutakuwa urahisi wa kufanya hivo - la sivyo atangulize mikono yake kabla ya magoti yake. Vidole vya miguu na mikono yake vinatakiwa kuelekea Qiblah na vilevile aachanishe vidole vya mikono yake. Anatakiwa kusujudu juu ya viungo vyake saba: paji la uso, pua, mikono yake miwili, magoti yake mawili na matumbo ya vidole vya miguu yake. Halafu aseme:

"Subhaana Rabbiy´ al-A´laa"

"Utakasifu ni wa Mola, Aliye juu."

Akariri hivo mara tatu au zaidi.

Imependekezwa kuongezea juu yake:

"Subhaanaka, Allaahumma Rabbanaa wa bihamdik. Allaahumma Ighfir liy."

"Ee Mola! Utakasifu na himdi zote ni Zako. Ee Allaah! Nisamehe." (al-Bukhaariy (761), Muslim (484), an-Nasaa´iy (1122), Abu Daawuud (877), Ibn Maajah (889) na Ahmad (06/43).)

Vilevile aombe du´aa kwa wingi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)

amesema:

"Katika Rukuu´ muadhimisheni Mola. Ama katika Sujuud jitahidini katika kuomba du´aa, kwani kuna matarajio mkaitikiwa."(Muslim (738), Abu Daawuud (742), Ahmad (1260) na (1801).)

Ajiombee kwa Mola Wake yeye du´aa na awaombee vilevile waislamu wengine mema ya duniani na ya Aakhirah. Afanye hivi sawa katika swalah ya faradhi na ya Sunnah. Anatakiwa vilevile kutanua mikono yake mbali na mbavu zake, tumbo mbali na mapaja yake, mapaja mbali na miguu yake na asiinamishe mikono yake juu ya ardhi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

"Nyookeni katika Sujuud na wala mmoja wenu asiinamishe mikono yake kama inavyofanya mbwa."(al-Bukhaariy (779), Muslim (762) na an-Nasaa´iy (1098).)