´Aqiydah Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah
Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn

Matunda ya ´Aqiydah hii

´Aqiydah hii ya kimbingu, ilio na misingi hii mikubwa, inampa mwenye nayo matunda mengi mazuri.

Kumuamini Allaah (Ta´ala) na Majina na Sifa Zake, kunamfanya mja kumpenda Allaah na kumuadhimisha. Kunampelekea yeye kutekeleza maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake. Kwa hayo kunapatikana kwa mtu binafsi na jamii furaha kamilifu duniani na Aakhirah.

"Mwenye kutenda mazuri miongoni mwa wanamume au wanawake naye ni Muumin, Tutamhuisha uhai mzuri, na bila shaka Tutawalipa ujira wao kwa mazuri zaidi ya yale waliyokuwa wakitenda." (16:97)

Matunda yanayopatikana kwa kuwaamini Malaika, ni pamoja na yafuatayo:

1. Ujuzi juu ya Ukubwa wa Muumbaji Wao (Tabaarak wa Ta´ala), Uwezo Wake na Nguvu Zake.

2. Kumshukuru (Ta´ala) kwa kuwajali waja Wake. Amewawakilisha Malaika hawa kuwahifadhi, kuandika matendo yao na maslahi yao mengine.

3. Kuwapenda Malaika kutokana na ´ibaadah wanazomfanyia Allaah (Ta´ala) kwa njia timilifu na kuwaombea kwao msamaha waumini.

Miongoni mwa matunda yanayopatikana kwa kuamini Vitabu, ni pamoja na yafuatayo:

1. Ujuzi wa kumjua Allaah (Ta´ala) na namna anavyowajali waja Wake kwa vile ameteremsha Kitabu kwa kila Ummah ambacho anawaongoza kwacho.

2. Dalili ya Hekima ya Allaah (Ta´ala) pale ambapo ameweka katika Vitabu hivi kwa kila Ummah yale yenye kuendana na wao. Kitabu cha mwisho katika Vitabu hivi ni Qur-aan Kubwa na inaendana na viumbe wote katika kila zama na mahala mpaka siku ya Qiyaamah.

3. Kushukuru neema ya Allaah (Ta´ala) juu ya hilo.

Miongoni mwa matunda yanayopatikana kwa kuamini Mitume, ni pamoja na yafuatayo:

1. Ujuzi wa kujua Huruma wa Allaah (Ta´ala) na kuwa anawajali viumbe Wake kwa kuwatumia Mitume watukufu kwa ajili ya uongofu na maelekezo.

2. Kumshukuru Allaah (Ta´ala) kwa neema hii kubwa.

3. Kuwapenda Mitume, kuwaadhimisha na kuwasifu kwa njia inayotakikana. Pamoja na yote wao ni Mitume wa Allaah (Ta´ala) na waja wasafi.

Wamemuabudu Allaah, kufikisha ujumbe Wake, kuwanasihi waja Wake na kuvumilia maudhi yao.

Miongoni mwa matunda yanayopatikana kwa kuamini siku ya Mwisho, ni pamoja na yafuatayo:

1. Kupupia kumtii Allaah (Ta´ala) kwa malengo ya kulipwa siku hiyo na kujiepusha na kumuasi kwa kukhofia kuadhibiwa siku hiyo.

2. Muumini kuliwazika na furaha na vipumbazo vya duniani vinavyompita kutokana na neema na malipo ya Aakhirah anayoyatarajia.

Miongoni mwa matunda yanayopatikana kwa kuamini Qadar, ni pamoja na yafuatayo:

1. Kumtegemea Allaah (Ta´ala) pindi kunapotokea jambo, kwa kuwa sababu na chenye kusababishwa yote mawili yanatokamana na mipango na makadirio ya Allaah (Ta´ala).

2. Nafsi yenye raha na utulivu wa moyo. Pindi mtu anapojua kuwa mambo yote yanatokamana na aliyoyapanga Allaah (Ta´ala) na kuwa yanayochukiwa ni lazima yapitike, nafsi inapata starehe na moyo unapata utulivu na kuridhia maamuzi ya Mola. Hakuna mwenye maisha mazuri kabisa, moyo wenye raha na utulivu mkubwa kabisa kama yule mwenye kuamini Qadar.

3. Mtu asijione pindi anapopata kitu maalum, kwa sababu kupata kitu hicho kunatokamana na neema ya Allaah. Hivyo amshukuru Allaah na aache majivuno.

4. Mtu kutokuwa na wasiwasi na kuhuzunika pindi anapokosa kitu maalum au kufikwa na kitu chenye kuudhi. Yote hayo yanatokamana na mipango ya Allaah (Ta´ala), Mola wa mbingu na ardhi. Yaliyopangwa ni lazima yapitike na hakuna namna ya kuyazuia. Kwa ajili hiyo awe na subira juu ya hilo na atarajie malipo.

Haya ndio anayoashiria Allaah (Ta´ala) pale anaposema:


“Hakuna msiba wowote unaokusibuni katika ardhi au katika nafsi zenu isipokuwa umo katika Kitabu kabla Hatujauumba [huo msiba] - hakika hayo kwa Allaah ni mepesi. Ili msisononeke juu ya yale yaliyokuondokeeni na wala msifurahie kwa yale Aliyokupeni; na Allaah Hapendi kila mwenye kujinata, anayejifakharisha.” (57:22-23)

Tunamuomba Allaah (Ta´ala) atuthibitishe katika ´Aqiydah hii, atutunukie matunda yake, atuzidishe katika fadhila Zake, asizipotoshe nyoyo zetu baada ya kuziongoza na aturehemu - hakika Yeye ndiye mwenye kutoa - himdi zote ni Zake Allaah, Mola wa walimwengu.

Swalah na salaam zimwendee Mtume wetu Muhammad, familia yake, Maswahabah zake na wenye kuwafuata kwa wema.