´Aqiydah Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah
Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn

Kuwaamini Malaika

Tunawaamini Malaika wa Allaah (Ta´ala) na kwamba:

“Ni waja waliokirimiwa. Hawamtangulii [Allaah] kwa kauli, nao kwa amri Yake wanafanya." (21:26-27)

Allaah (Ta´ala) amewaumba na wanamuabudu na kumtii kwa kumnyenyekea:

"Hawatakabari na ‘ibaadah Yake na wala hawachoki. Wanamtukuza usiku na mchana, wala hawazembei." (21:19-20)

Allaah ametuficha nao na kwa ajili hiyo hatuwaoni. Hata hivyo kuna uwezekano baadhi ya waja wakawaona. Kwa mfano Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona Jibriyl (´alayhis-Salaam) katika umbile lake la asli. Alikuwa na mbawa mia sita zilizokuwa zimefunika upeo wa juu wote.

Kadhalika alijifananisha katika umbile sawa na mtu wakati alipomshukia Maryam. Jibriyl akazungumza naye na Maryam na yeye akazungumza naye. Vilevile siku moja alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake katika umbile la mtu. Walikuwa hawamjui mtu huyo; hakuwa na alama yenye kuonesha kuwa ni msafiri na alikuwa na nguo nyeupe pee na nywele zake zilikuwa nyeusi sana. Akakaa kandoni na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), akaweka magoti yake karibu na magoti ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akaweka vitanga vyake juu ya magoti yake. Akazungumza na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akazungumza naye. Baada ya hapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawaeleza Maswahabah zake ya kwamba mtu yule alikuwa ni Jibriyl.

Tunaamini kuwa Malaika wamelazimishwa kazi mbali mbali. Jibriyl amewakilishwa kuteremsha Wahyi kuutoa kwa Allaah na kumteremshia Nabii na Mtume amtakaye. Mikaaiyl amewakilifishwa mvua na mazao.

Israafiyl amewakilishwa kupuliza baragumu itapofika wakati wa Kuzimia na Kufufuliwa.

Malaika wa mauti amewakilishwa kuzichukua roho za watu inapofika wakati wa mauti.

Malaika wa mlima amewakilishwa na mlima.

Malaika Maalik ambaye ni mlinzi wa Moto.

Kuna Malaika waliowakilishwa na vipomoko kwenye vifuko vya uzazi. Kuna Malaika wengine wamewakilishwa kumhifadhi mwanaadamu, wengine wamewakilishwa kuandika matendo yao, kwa sababu kila mtu ana Malaika wawili:


“Pale wanapopokea wapokeaji wawili wanaokaa kuliani na kushotoni. Hatamki kauli yeyote ile isipokuwa yuko karibu naye mwangalizi amejitayarisha [kurekodi].” (50:17-18)

Kadhalika kuna Malaika waliowakilishwa kumuhoji maiti. Pale ambapo maiti ameshawekwa kwenye mwana-ndani, anajiwa na Malaika wawili na wanamuuliza kuhusu Mola Wake, dini Yake na Mtume Wake.


"Allaah Huwathibitisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika uhai wa dunia na Aakhirah. Na Allaah Huwaacha kupotoka madhalimu. Na Allaah Anafanya Atakavyo." (14:27)

Kuko Malaika waliowakilishwa na watu wa Peponi:


"Na Malaika wanawaingilia katika kila milango [na kusema] “Salaamun ‘Alaykum” [Amani iwe juu yenu] kwa yale mliyosubiri. Basi uzuri ulioje hatima [nzuri] ya nyumba [ya Aakhirah]." (13:23-24)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameeleza kuwa Nyumba inayozuriwa mbinguni huingia (na katika upokezi mwingine "huswali ndani yake”) kwa kila siku moja Malaika elfu sabini kisha baada ya hapo hakuna katika wao anayerudi tena.