´Aqiydah Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah
Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn

Kumuamini Allaah

Yote tuliyoyataja kuhusiana na Sifa za Allaah (Ta´ala), kwa ufafanuzi au kwa jumla, kuthibitisha au kukanusha, ni wenye kutegemea Kitabu cha Mola Wetu na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa mujibu wa ufahamu wa wahenga wa Ummah huu, maimamu wa Uongofu na wafuasi wao.

Kuhusiana na suala hili, tunaona kuwa ni wajibu kuyapitisha/kuyafasiri maandiko ya Qur-aan na Sunnah kwa udhahiri wake na kuyaamini uhakika wake kwa njia yenye kulingana na Allaah (´Azza wa Jall).

Tunajitenga mbali na msimamo wa wale watu wenye msimamo wa kuyapindisha.

Wameyefasiri kwa njia nyingine mbali na ile aliyokusudia Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Vilevile tunajitenga mbali na wale watu waliyoyakanusha kwa ile maana aliyokusudia Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kadhalika tunajitenga mbali na wale watu waliyoyafasiri kwa njia yenye kuvuka mipaka na wakawa ima wameyafananisha au kuyawekea namna.

Tunajua kwa yakini ya kwamba yale yote yaliyokuja katika Kitabu cha Allaah (Ta´ala) au Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni haki na hayagongani:

"Je hawaizingatii Qur-aan? Na lau ingelikuwa imetoka kwa mwingine asiyekuwa Allaah, bila shaka wangelikuta ndani yake tofauti nyingi." (04:82)

Kupatikana mgongano humo, kunalazimisha baadhi ya maandiko kukadhibisha mengine - na hili ni jambo lisilowezekana katika maelezo ya Allaah (Ta´ala) na maelezo ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mwenye kudai kuwa katika Kitabu cha Allaah au Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuna kitu kujigonga, hilo linatokamana na makusudio yake mabaya na ni kwa sababu ana moyo uliyopinda. Kwa ajili hiyo anatakiwa kutubu kwa Allaah (Ta´ala) au kuigeuzia dhambi yake mgongo.

Hata hivyo yule mwenye kufikiri kuwa katika Kitabu cha Allaah (Ta´ala), Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au kati yavyo viwili kuna mgongano, hilo linatokamana ima na udogo wa elimu yake, ufahamu wake mpungufu au ufupi wa kuzingatia kwake. Kwa hivyo mtu kama huyo anatakiwa kutafuta elimu na azingatie kwa kina mpaka haki iweze kumbainikia. Ikiwa mambo hayakumbainikia, basi ampasie jambo hilo mwalimu wake, akomeke na fikira zake na aseme yale wanayosema waliobobea katika elimu:


“Tumeziamini, zote ni kutoka kwa Mola wetu.” (03:07)

Pamoja na hivyo anatakiwa kujua kuwa katika Qur-aan na Sunnah hakuna kabisa hakujigonga na hii haigongi nyingine wala hakuna kutofautiana kati yavyo.