´Aqiydah Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah
Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn

Kuamini Vitabu

Tunaamini kuwa Allaah (Ta´ala) ameteremsha Vitabu ambavyo ni hoja dhidi ya viumbe na ni hoja kwa waumini. Kwavyo, wanawafunza hekima na kuwatakasa.

Tunaamini kuwa Allaah (Ta´ala) amemteremshia kila Mtume Kitabu. Amesema (Ta´ala):


“Kwa yakini Tuliwapeleka Mitume Wetu kwa hoja bayana na Tukateremsha pamoja nao Kitabu na mizani ili watu wasimamie uadilifu.” (57:25)

Miongoni mwa Vitabu hivyo tunajua vifuatavyo:

1. Tawraat ambayo Allaah (Ta´ala) amemteremshia Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Tawraat ndio Kitabu kikubwa kwa wana wa Israaiyl.


"Humo mna mwongozo na nuru ambayo kwayo, Manabii waliojisalimisha [kwa Allaah] waliwahukumu Mayahudi na watawa na wanazuoni wa kiyahudi pia [walihukumu kwa hiyo Tawraat] kwa sababu waliyokabidhiwa kuhifadhi Kitabu cha Allaah; na wakawa mashahidi juu yake." (05:44)

2. Injiyl ambayo Allaah (Ta´ala) amemteremshia ´Iysaa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Inaisadikisha Tawraat na kuikamilisha.


"Na Tukampa Injiyl iliyomo ndani yake mwongozo na nuru; na isadikishayo yale yaliyokuwa kabla yake katika Tawraat, na ni mwongozo na mawaidha kwa wenye taqwa." (05:46-47)

"Ili nikuhalalishieni baadhi ya yale yaliyoharamishwa kwenu." (03:50)

3. Zabuur ambayo Allaah (Ta´ala) amempa Daawuud (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

4. Suhuf ya Ibraahiym na Muusa (´alayhimaas-Salaam).

5. Qur-aan Kubwa ambayo Allaah (Ta´ala) amemteremshia Mtume wa mwisho Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).


"Ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo." (02:185)


"Kinachosadikisha yale [yaliyokuja katika] Vitabu vilivyokuwa kabla yake na kuvihukumia." (05:48)

Allaah amevifuta Vitabu vyote vilivyotangulia kwa Qur-aan na Akachukua jukumu la kuihifadhi na mchezo wa wachezaji na upindaji wa wapindaji.


"Hakika Sisi ndio Tumeteremsha Ukumbusho [huu] na Sisi bila shaka ndio Tutakaoihifadhi." (15:09)

Itaendelea kubaki kuwa ni hoja juu ya viumbe vyote mpaka siku ya Qiyaamah. Ama kuhusu Vitabu vilivyotangulia, ni vya muda fulani mpaka kunaposhuka Uteremsho wenye kuvifuta na kubainisha yaliyopotoshwa humo na kubadilishwa. Kwa ajili hiyo ndio maana havikuhifadhiwa na hivyo
vikapotoshwa, vikazidishwa na kupunguzwa:


"Katika Mayahudi wako wanaobadilisha maneno kuyatoa mahali pake" (04:46)


"Basi ole kwa wale wenye kuandika kitabu kwa mikono yao; kisha wakasema: ”Haya ni kutoka kwa Allaah” ili wayabadilishe kwa thamani ndogo. Basi ole wao kwa yale yaliyoandikwa na mikono yao, na ole wao kwa yale wanayoyachuma." (02:79)

“Nani aliyeteremsha Kitabu ambacho amekuja nacho Muwsaa, [chenye] nuru na mwongozo kwa watu. Mnakifanya kurasa kurasa mkizifichua na mkificha mengi." (06:91)


"Na hakika miongoni mwao kuna kundi wanaopinda ndimi zao kwa [kusoma] Kitabu ili mdhanie kuwa hayo ni yanayotoka katika Kitabu na hali hayo si yenye kutoka katika Kitabu, na wanasema: “Hayo ni kutoka kwa Allaah”; na hali hayo si kutoka kwa Allaah na wanamsingizia uongo Allaah na wao wanajua. Haiwi kwa mtu [aliye Rasuli] kwamba Allaah Amempa Kitabu na hukumu na Unabii kisha awaambie watu: “Kuweni wenye kuniabudu mimi badala ya Allaah” (03:78-79)


"Enyi watu wa Kitabu! Hakika amekwishakujieni Mtume Wetu anayekubainishieni mengi katika yale mliyokuwa mkiyaficha katika Kitabu." (05:15)


"Kwa yakini wamekufuru wale waliosema: “Hakika Allaah Ndiye al- Masiyh mwana wa Maryam.” (05:17)