´Aqiydah Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah
Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
Kuamini siku ya Qiyaamah
Tunaamini siku ya Mwisho ambayo ni siku ya Qiyaamah. Hakuna siku baada yake. Siku hiyo watu watafufuliwa ilihali wako hai kwa ajili ya maisha ya milele. Makazi yao ya mwisho itakuwa ima ni Peponi au Motoni.
Tunaamini Kufufuliwa ambapo Allaah atawahuisha maiti. Hili litapitika pale ambapo Israafiyl atapopuliza baragumi kwa mara ya pili:
"Na itapulizwa baragumu; watazimia wale walioko mbinguni na ardhini isipokua Amtakaye Allaah. Kisha litapulizwa humo mara nyingine, tahamaki hao wanasimama wakitazama." (39:68)
Watu watainuka kutoka kwenye makaburi yao kwa ajili ya Mola wa walimwengu. Watakuwa miguu peku, uchi na bila ya kutahiriwa:

"Kama Tulivyoanza [uumbaji] umbo la awali Tutalirudisha. Hii ni ahadi juu Yetu. Hakika Sisi Tumekuwa ni Wenye kufanya [Tuyasemayo]." (21:104)
Tunaamini Madaftari ya matendo. Yatagawiwa kwa mkono wa kulia au nyuma ya mgongo [upande wa] kushoto:
“Basi ama yule atakayepewa kitabu chake kuliani mwake, basi atahesabiwa hesabu nyepesi na atageuka kwa ahli zake akiwa mwenye furaha. Na ama yule atakayepewa kitabu chake nyuma ya mgongo wake, basi ataomba maangamizi na ataingia aungue [Moto wa] Sa’iyraa.” (84:07-12)
"Na kila mwanaadamu Tumemuambatanishia majaaliwa ya ‘amali zake shingoni mwake. Na Tutamtolea Siku ya Qiyaamah kitabu atakachokikuta kimekunjuliwa. [Ataambiwa]: “Soma kitabu chako! Nafsi yako inakutosheleza leo kukuhesabia dhidi yako.” (17:13-14)
Tunaamini Mizani itayowekwa siku ya Qiyaamah na hakuna yeyote atayedhulumiwa:

“Basi yule atakayetenda kheri uzito wa chembe ya atomu basi ataiona. Na yule atakayetenda shari uzito wa chembe ya atomu basi ataiona.” (99:07-08)

"Basi yule ambaye mizani yake itakuwa nzito, hao ndio wenye kufaulu. Na yule ambaye mizani yake itakuwa khafifu, basi hao ni wale ambao zimekhasirika nafsi zao, [watakuwa] katika [Moto wa] Jahannam ni wenye kudumu. Moto utababua nyuso zao; nao humo [watakuwa] ni wenye nyuso zilizokunjana." (23:102-104)
"Afanyae wema atalipwa mfano wake mara kumi. Na afanyae ubaya hatalipwa isipokuwa sawa nao tu na wao hawatadhulumiwa." (06:160)
Tunaamini Uombezi mkubwa ambao itakuwa ni haki ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) peke yake. Baada ya Allaah kumpa idhini, atashufaia kwa Allaah ili viumbe wafanyiwe hesabu.
Watakuwa na hali ngumu wasiyoiweza. Wataanza kwenda kwa Aadam, kisha Nuuh, kisha Ibraahiym,
kisha Muusa, kisha ´Iysaa mpaka mwishoni waende kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).
kisha Muusa, kisha ´Iysaa mpaka mwishoni waende kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).
Tunaamini kuwepo uombezi kwa wale waumini walioingia Motoni watolewe.
Uombezi huu ni kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Mitume wengine, waumini na Malaika.
Vilevile tunaamini kuwa Allaah atawatoa watu kutoka Motoni kutokana na
Fadhila na Huruma Wake pasi na uombezi wowote. Tunaamini hodhi ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Maji yake ni meupe zaidi kuliko maziwa, matamu zaidi kuliko asali na yenye kunukia vizuri zaidi kuliko miski. Urefu wake na upana wake ni sawa na mwendo wa safari ya mwezi. Vikombe vyake ni vizuri sana na vingi kama nyota za mbinguni.
Waumini katika Ummah wake ndio wataiendea. Atakayekunywa mara moja hatopata kiu tena baada ya hapo.
Tunaamini Njia ilioko juu ya Moto. Watu watapita juu yake kutegemea na matendo yao. Wa kwanza wao atapita kama umeme, wa pili atapita kama upepo, ndege au ngamia. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) atakuwa amesimama juu ya Njia na huku anasema:
"Ee Mola! Salimisha, salimisha."
Matendo ya waja yataisha na hapo ndipo watakuja baadhi hali ya kuwa wanatambaa. Kwenye ncha ya Njia kuna miba ilioamrishwa kumwangusha yule iliyoamrishwa. Mwenye furaha ataokoka na mwangamivu atatumbukia Motoni.
Tunaamini yale yote yaliyotajwa katika Qur-aan na Sunnah kuhusiana na siku hii na hali zake - tunamuomba Allaah atusaidie kwazo.
Tunaamini uombezi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa watu wa Peponi waingie.
Uombezi huu ni maalum kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).
Tunaamini Pepo na Moto. Pepo ni makazi ya starehe ambayo Allaah amewaandalia waumini wenye kumcha. Humo mna neema ambazo hakuna yeyote ameshawahi kuziona, kuzisikia wala kujifikiria nazo.

"Nafsi yoyote haijui yaliyofichiwa katika yanayoburudisha macho. Ni jazaa kwa yale waliyokuwa wakiyatenda." (32:17)
Moto ni makazi ya adhabu ambayo Allaah (Ta´ala) amewaahidi makafiri madhalimu. Humo mna adhabu isiyoweza kufikiriwa.
"Hakika Sisi Tumewaandalia madhalimu Moto ambao kuta zake zitawazunguka. Na wakiomba msaada watasaidiwa kwa [kupewa] maji kama mafuta meusi ya moto yanayobabua nyuso. Ubaya ulioje kinywaji hicho, na uovu ulioje mahali pa kupumzikia." (18:29)
Vinapatikana hivi sasa na havitotoweka hata siku moja.

“Na yeyote [yule] anayemwamini Allaah na akatenda [‘amali] njema, [basi Allaah] Atamuingiza mabustani yapitayo chini yake mito ni wenye kudumu humo milele - Allaah Amekwishampa riziki nzuri.” (65:11)

"Hakika Allaah Amewalaani makafiri na Amewaandalia [Moto wa] Sa’iyraa. Ni wenye kudumu humo milele. Hawatopata mlinzi na wala mwenye kunusuru. Siku zitakapopinduliwa nyuso zao Motoni, watasema: “Laiti tungelimtii Allaah na tungelimtii Mtume.” (33:64-66)
Tunashuhudia Pepo juu ya kila ambaye Qur-aan na Sunnah vimemtolea ushahidi, sawa ikiwa ni mtu kwa dhati yake au kwa maelezo. Waliopewa ushahidi kwa dhati zao ni pamoja na Abu Bakr, ´Umar, ´Uthmaan, ´Aliy na wengine ambao Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwateua kwa dhati
zao. Miongoni mwa zile sifa zilizotolewa ushahidi ni ushahidi wa imani ya muumini na uchaji Allaah wa mwenye kumcha.
zao. Miongoni mwa zile sifa zilizotolewa ushahidi ni ushahidi wa imani ya muumini na uchaji Allaah wa mwenye kumcha.
Tunamshuhudia Moto kila ambaye Qur-aan na Sunnah vimemtolea ushahidi, sawa ikiwa ni mtu kwa dhati yake au kwa maelezo. Waliopewa ushahidi kwa dhati zao ni pamoja na Abu Lahab, ´Amr bin Luhayy al-Khuzaa´iy na wengineo.
Miongoni mwa zile sifa zilizotolewa ushahidi ni ushahidi wa kufuru ya kafiri, shirki kubwa ya mshirikina na unafiki wa mnafiki.
Tunaamini fitina ya kaburi ikiwa na maana ya kwamba maiti ataulizwa kuhusu Mola, dini na Mtume Wake.

"Allaah Huwathibitisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika uhai wa dunia na Aakhirah." (14:27)
Muumini atasema:
"Mola wangu ni Allaah, Uislamu ndio dini yangu na Muhammad ndio Mtume wangu."
Kuhusu kafiri na mnafiki watasema:
"Sijui. Niliwasikia watu wakisema kitu na mimi nikakisema."
Tunaamini kuwa waumini wataneemeshwa ndani ya makaburi:

"Ambao Malaika huwafisha katika hali nzuri [Malaika] watasema: [kuwaambia Waumini]: “Salaamun ‘Alaykum [amani iwe juu yenu]! Ingieni Peponi kwa yale mliyokuwa mkitenda.” (16:32)
Tunaamini kuwa madhalimu na makafiri wataadhibiwa ndani ya makaburi:

"Na lau ungeliona madhalimu pale wakiwa katika mateso makali ya mauti, na Malaika wamenyosha mikono yao [wakiwaambia]: “Zitoeni nafsi zenu! Leo mnalipwa adhabu ya kudhalilisha kwa yale mliyokuwa mkiyasema juu ya Allaah pasi na haki na kwa vile mlivyokuwa mkifanya kiburi juu ya Aayaat Zake." (06:93)
Ahaadiyth kuhusiana na suala hili ni nyingi na zinajulikana. Ni lazima kwa muumini kuamini yale yote yaliyokuja katika Qur-aan na Sunnah juu ya mambo haya yenye kufichikana, pasi na kuyalinganisha na yale anayoyaona duniani.
Mambo ya Aakhirah hayawezi kulinganishwa na mambo ya duniani, kwa
sababu kuna tofauti kubwa kati ya hayo mawili.
sababu kuna tofauti kubwa kati ya hayo mawili.