´Aqiydah Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah
Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
Kuamini Qadar
Tunaamini Qadar, kheri na shari yake. Allaah amepanga makadirio ya viumbe kwa mujibu wa utanguliaji wa Ujuzi Wake na kutokana na vile Hekima Yake inavyopelekea.
Qadar ina ngazi nne:
1. Ujuzi. Tunaamini kuwa Allaah (Ta´ala) juu ya kila kitu ni Mjuzi. Kwa Elimu Yake ya milele na yenye kudumu anayajua yaliyokuwepo, yatayokuwepo na namna yatavyokuwepo. Katika Elimu Yake hakuna kitu kinachokuwa kipya baada ya kutokukijua na Elimu Yake haifikiwi na kitu kusahau.
2. Uandishi. Tunaamini kuwa Allaah (Ta´ala) ameandika kwenye Ubao uliohifadhiwa yatayokuwepo mpaka siku ya Qiyaamah:

"Je, huelewi kwamba Allaah Anajua yale yote yaliyomo katika mbingu na ardhi? Hakika hayo yamo katika Kitabu. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi." (22:70)
3. Utashi. Tunaamini kuwa kila kilichopo mbinguni na ardhini kinapitika kwa matakwa ya Allaah (Ta´ala). Hakukuwi kitu isipokuwa kwa Kutaka Kwake. Kile anachokitaka Allaah ndio huwa, na kile asichokitaka hakiwi.
4. Uumbaji. Tunaamini kuwa:

"Allaah ni Muumbaji wa kila kitu, Naye juu ya kila kitu ni Mtegemewa.
Pekee Anazo funguo za mbingu na ardhi." (39:62-63)
Pekee Anazo funguo za mbingu na ardhi." (39:62-63)
Ngazi hizi nne zinawakilishwa na yale anayofanya Allaah (Ta´ala) na waja. Allaah anajua yale yote wanayoyasema waja, wanayoyafanya au kuyaacha.
Anayaandika Kwake Mwenyewe (Ta´ala), Ameyataka na Kuyaumba:

“Kwa yule atakaye miongoni mwenu anyooke [katika njia ya haki]. Na hamtotaka isipokuwa Atake Allaah Mola wa walimwengu.” (81:28-29)

"Na lau Allaah Angetaka wasingeliyafanya hayo. Basi waachilie mbali na [hayo] wanayoyatunga."(06:137)
“Na hali Allaah Amekuumbeni na yale (yote) mnayoyafanya." (37:96)

Lakini pamoja na hivyo, tunaamini kuwa Allaah (Ta´ala) amemjaalia mja kuwa na khiyari na uwezo wa kutenda.
Dalili zifuatazo zinaonesha kuwa mja ana uhuru na uwezo wa kutenda:
1. Amesema (Ta´ala):

"Basi ziendeeni konde zenu vyovyote mpendavyo." (02:223)
"Na lau wangelitaka kutoka [kwenda vitani], wangeliandaa maandalizi yake." (09:46)

Amethibitisha kuwa waja wanaweza kwenda kwa kutaka kwao na kufanya maandalizi kwa utashi wao.
2. Mja ameelekezwa maamrisho na makatazo. Lau asingekuwa na utashi wa khiyari na uwezo, basi angelikuwa ameelekezwa katika kitu asichoweza kukifanya. Ni kitu chenye kukataliwa na Hekima ya Allaah (Ta´ala), huruma Wake na maelezo Yake ya kweli:

3. Mwenye kufanya kitendo chema anasifiwa na mwenye kufanya kitendo kiovu analaumiwa. Kila mmoja analipwa kwa njia anayoistahiki. Lau ingelikuwa kitendo hakipitiki kwa utashi wa khiyari ya mja, kumsifu mwenye kufanya kitendo chema kungelikuwa hakuna maana yoyote na kumlaumu mwenye kufanya kitendo kiovu ingelikuwa ni dhuluma.
4. Allaah amewatuma Mitume:

"Mitume ni wabashiriaji na waonyaji ili pasikuweko kutoka kwa watu hoja yoyote juu ya Allaah baada ya [kuletwa] Mitume."(04:165)
Lau mja angelikuwa ni mwenye kutenda pasi na kupenda na kutaka kwake, hoja yake ingelikuwa si yenye kubatilika baada ya kutumwa Mitume.
5. Kila mwenye kutenda au kukiacha kitu, anahisi kuwa amekifanya bila ya kutenzwa nguvu.
Anasimama, anakaa, anaingia, anatoka na anasafiri kwa kutaka kwake. Hahisi kabisa kuwa kuna yeyote mwenye kumlazimisha kufanya hayo.
Anatofautisha wazi wazi baina ya anapofanya kitu kwa khiyari yake na pindi anapolazimishwa. Hali kadhalika Shari´ah imetofautisha kati ya hayo mawili kwa njia ya busara. Mlazimishwaji haadhibiwi kwa kitu alichotenzwa nguvu, ikiwa kitendo hicho kinahusiana na haki ya Allaah (Ta´ala).
Tunaona kuwa mtenda dhambi hana hoja yoyote kwa dhambi yake kutokana na Qadar ya Allaah (Ta´ala). Mtenda dhambi anafanya dhambi kwa khiyari yake bila ya kujua kuwa Allaah (Ta´ala) amemkadiria nayo, kwa sababu hakuna yeyote anayejua makadirio ya Allaah (Ta´ala) isipokuwa baada ya kutokea kilichopangwa:

"Na nafsi yoyote haijui nini itachuma kesho." (31:34)
Vipi basi itakuwa ni sahihi kwa mtu huyu kutumia hoja kwa kitu ambacho yeye mwenyewe hajui kinapelekea katika nini? Allaah (Ta´ala) amebatilisha hoja hii kwa Kauli Yake:

"Watasema wale walioshirikisha: “Lau Allaah Angetaka tusingelifanya shirki, wala baba zetu [wasingelishirikisha pia] na wala tusingeliharamisha chochote.” Hivyo ndivyo walivyokadhibisha wale wa kabla yao mpaka walipoonja adhabu Yetu. Sema: “Je, mna elimu yoyote mtutolee? Hamfuati isipokuwa dhana tu, nanyi si lolote ila mnabuni uongo.” (06:148)
Tunamwambia mtenda dhambi ambaye anailaumu Qadar yafuatayo:
Kwa nini hukufanya kitendo chema kwa kukadiria ya kwamba Allaah (Ta´ala) amekupangia nacho? Hakuna tofauti kati yacho na kati ya dhambi inayofanywa kwa kutokujua yaliyopangwa kabla ya kutokea kwake.
Kutokana na sababu hiyo wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipowaambia Maswahabah ya kwamba kila mmoja ameshaandikiwa mahali pake Peponi au Motoni.
Wakasema: "Situache kutenda na tutegemee hayo?"
Akajibu: "Hapana, tendeni, hakika kila mmoja amesahilishiwa kwa yale aliyoumbiwa kwayo."
Tunamwambia mtenda dhambi ambaye anailaumu Qadar yafuatayo:
Hebu tuchukulie unataka kusafiri kwenda Makkah na uko na njia mbili. Mtu mwaminifu akakueleza kuwa njia moja ni ya khatari na ngumu, na njia nyingine ni ya usalama na nyepesi. Hapa utachukua hii ya pili. Ni jambo lisilowezekana ukachukua ile ya kwanza na kusema: "Imeshakadiriwa kwangu." Lau utafanya hivo, watu watachukulia kuwa ni mwendawazimu.
Tunasema pia:
Tuseme kuwa umepewa kazi mbili. Moja katika kazi hizo ina mshahara mnono.
Vipi basi utaweza kuchagua kazi ilio na mshara wa chini halafu uilaumu Qadar?
Tunasema kumwambia tena:
Tuchukulie kuwa umesibiwa na maradhi ya kimwili. Unabisha hodi mlango wa kila daktari ili kujitibisha. Unavumilia maumivu baada ya upasuaji na madawa machungu. Ni kwa nini basi usifanye vivyo hivyo kwa moyo wako ulio mgonjwa kwa madhambi?
Tunaamini kuwa shari hainasibishwi kwa Allaah (Ta´ala) kutokana na ukamilifu wa Huruma na Hekima Yake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
"Shari haitoki Kwako."
Ameipokea Muslim.
Maamuzi ya Allaah (Ta´ala) yenyewe sio shari, kwa sababu yametokamana na huruma na hekima. Hata hivyo shari inaweza kuwa katika yale yaliyoamuliwa.
Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kwenye du´aa ya Qunuut aliyoamfunza al-Hasan:
"Nilinde na shari Uliyoamua."
Amefungamanisha shari na yale Aliyoyaamua. Pamoja na hivyo, shari katika yaliyopangwa sio shari ilio safi na ilio tupu. Bali ni shari kwa mtazamo fulani na ni kheri kwa mtazamo mwingine. Ufisadi unaotokea katika ardhi wa ukame, maradhi, ufakiri na khofu ni shari, lakini vilevile ni kheri kwa mtazamo mwingine. Allaah (Ta´ala) amesema:

"Ufisadi umedhihiri katika nchi kavu na baharini kwa sababu ya yale iliyochuma mikono ya watu ili Awaonjeshe baadhi ya ambayo wameyatenda ili wapate kurejea [kutubu]." (30:41)
Kukata mkono wa mwizi na kumpiga mawe mzinifu ni shari kwa nisba ya mtendaji, lakini ni kheri kwao kwa kuzingatia ya kwamba madhambi yao yanasamehewa. Hawatoadhibiwa duniani na Aakhirah. Hali kadhalika ni kheri kwa sababu kuna kuhifadhiwa kwa mali, heshima na ukoo.