´Aqiydah Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah
Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
Kuamini Mitume
Tunaamini kuwa Allaah (Ta´ala) amewatumia viumbe Wake Mitume:
"Mitume ni wabashiriaji na waonyaji ili pasikuweko kutoka kwa watu hoja yoyote juu ya Allaah baada ya [kuletwa] Mitume. Na Allaah daima ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika daima, Mwenye hikmah wa yote daima." (04:165)
Tunaamini kuwa wa mwanzo wao ni Nuuh na wa mwisho wao ni Muhammad
(Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):
(Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

"Hakika Tumekufunulia Wahy kama Tulivyomfunulia Wahy Nuwh na Manabii baada yake." (04:163)

"Hakuwa Muhammad baba wa mmoja yeyote miongoni mwa wanaume wenu, lakini ni Mtume wa Allaah na ni mwisho wa Manabii." (33:40)
Mbora wao wa kwanza ni Muhammad, kisha Ibraahiym, kisha Muusa, kisha Nuuh na halafu ´Iysaa, mwana wa Maryam. Wamekhusishwa katika Kauli Yake (Ta´ala):
"Na [kumbusha pale] Tulipochukua kutoka kwa Manabii fungamano yao na kutoka kwako, na kutoka kwa Nuwh, na Ibraahiym, na Muwsaa, na ‘Iysaa mwana wa Maryam; na Tukachukua kutoka kwao fungamano gumu." (33:07)
Tunaamini kuwa Shari´ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ina kheri zote inayopatikana katika Shari´ah za Mitume hawa wa kipekee. Amesema (Ta´ala):
“Amekuamuruni katika Dini yale Aliyomuusia kwayo Nuwh, na ambayo Tumekuletea Wahy na Tuliyomuusia kwayo Ibraahiym, na Muwsaa na ‘Iysaa kwamba: “Simamisheni Dini na wala msifarikiane ndani yake.” (42:13)
Tunaamini kuwa Mitume wote ni wanaadamu walioumbwa. Hawana sifa hata moja ya Uungu. Amesema (Ta´ala) kuhusiana na Nuuh, ambaye ndiye wa kwanza wao:

“Na wala sikuambieni kwamba mimi nina hazina za Allaah, na wala sijui ya ghayb na wala sikuambieni kwamba mimi ni Malaika." (11:31)
Allaah (Ta´ala) amemwamrisha Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye ndiye wa mwisho wao, aseme:

“Sikuambieni kuwa mimi nina hazina ya Allaah; na wala kwamba najua mambo ya ghayb na wala sikuambieni kuwa mimi ni Malaika." (06:50)

"Sema: “Siimilikii nafsi yangu manufaa yoyote wala dhara yoyote isipokuwa
Apendavyo Allaah." (07:188)
Apendavyo Allaah." (07:188)

“Sema: “Hakika mimi sikumilikieni dhara na wala uongofu.” (72:21)
Tunaamini kuwa ni waja miongoni mwa waja wa Allaah ambao Allaah (Ta´ala) amewakirimu kwa ujumbe. Amewasifu kuwa ni waja wenye upeo wa juu na kadhalika Amewasifu. Amesema kuhusiana na wa mwanzo wao, Nuuh:

"Kizazi [cha wale] Tuliowabeba pamoja na Nuwh [katika jahazi]! Hakika yeye alikuwa mja mwenye shukurani.” (17:03)
Amesema kuhusu wa mwisho wao, Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

"Amebarikika Yule Ambaye Ameteremsha Pambanuzi kwa mja Wake ili awe muonyaji kwa walimwengu." (25:01)
Kadhalika amesema kuhusu Mitume wengine:

"Na [taja] waja Wetu; Ibraahiym, na Is-haaq, na Ya’quwb, wenye nguvu na utambuzi." (38:45)

“Na taja mja Wetu Daawuwd mwenye nguvu, hakika yeye ni mwenye kurudia rudia kutubu [kwa Allaah]." (38:17)

"Na Takamtunuku Daawuwd [mtoto] Sulaymaan; uzuri ulioje wa mja! Hakika yeye ni mwenye kurudia rudia kutubia [Kwetu]." (38:30)
Vilevile amesema juu ya ´Iysaa, mwana wa Maryam:

“Yeye si chochote isipokuwa tu ni mja Tuliyemneemesha, na Tukamjaalia [kuwa ni] mfano kwa wana wa Israaiyl.” (43:59)
Tunaamini kuwa Allaah (Ta´ala) amekhitimisha ujumbe kwa ujumbe wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amemtuma kwa watu wote.
Amesema (Ta´ala):

"Sema: “Hakika mimi ni Mtume wa Allaah kwenu nyinyi nyote. [Allaah] Ambaye Pekee Anao ufalme wa mbingu na ardhi. Hakuna mungu wa haki ila Yeye - Anahuisha na Anafisha. Basi mwaminini Allaah na Mtume Wake, Nabii asiyejua kusoma na kuandika ambaye anamwamini Allaah na maneno Yake, na mfuateni ili mpate kuongoka.” (07:158)
Tunaamini kuwa Shari´ah yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni dini ya Uislamu ambayo Allaah (Ta´ala) amewaridhia nayo waja Wake. Allaah (Ta´ala) hakubali kutoka kwa yeyote dini isiyokuwa Uislamu. Amesema (Ta´ala):

"Hakika Dini mbele ya Allaah ni Uislamu." (03:19)

"Leo Nimekukamilishieni dini yenu na Nimekutimizieni neema Yangu na Nimekuridhieni kwenu Uislamu uwe dini yenu." (05:03)

"Na yeyote anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitokubaliwa kwake; naye katika Aakhirah atakuwa miongoni mwa waliokhasirika." (03:35)
Tunaona kuwa mwenye kudai kuwa Allaah anakubali dini nyingine mbali na Uislamu, kwa mfano uyahudi au unaswara, ni kafiri. Mtu huyo anatakiwa kutubia au auawe hali ya kuwa ni mwenye kuritadi, kwa sababu ameikadhibisha Qur-aan.
Tunaona kuwa mwenye kukanusha ujumbe wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba umetumilizwa kwa watu wote basi amewakanusha Mitume wote, hata yule Mtume ambaye atakuwa anadai kuwa anamuamini na kumfuata. Amesema (Ta´ala):

"Watu wa Nuwh walikadhibisha Mitume." (26:105)
Amesema kuwa wamewakadhibisha Mitume wote, pamoja na kuwa hakukutanguliwa kuwepo na Mtume kabla ya Nuuh:

"Hakika wale waliomkanusha Allaah na Mtume Wake; na wanataka kufarikisha baina ya Allaah na Mtume Wake na wanasema: “Tunaamini baadhi [ya Mitume] na tunawakanusha baadhi” na wanataka kuchukua njia iliyo baina [kati kati] ya hayo – hakika hao ndio makafiri wa kweli. Na Tumewaandalia makafiri adhabu ya kudhalilisha." (04:150-151)
Tunaamini kuwa hakuna Nabii yoyote baada ya Muhammad Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa hiyo yule mwenye kudai kuwa ni Nabii baada yake au akamsadikisha mwenye kuja na madai hayo, ni kafiri, kwa sababu anamkadhibisha Allaah, Mtume Wake na maafikiano ya waislamu.
Tunaamini kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ana makhaliyfah waongofu. Wamechukua uongozi baada yake na kuuongoza Ummah wake kwa ujuzi, propaganda na uongozi na mamlaka juu ya waislamu. Mbora wao ni Abu Bakr as-Swiddiyq. Yeye ndiye mwenye haki zaidi ya ukhaliyfah. Kisha anafuata ´Umar bin al-Khattwaab, ´Uthmaan bin ´Affaan na kisha ´Aliy bin Abiy Twaalib
(Radhiya Allaahu ´anhum).
(Radhiya Allaahu ´anhum).
Namna hii ndivyo zilivyo fadhila zao, na pia ndivyo ustahiki wao wa kuongoza ulivyo. Allaah (Ta´ala) - na Yeye ana Hekima kubwa - katu asingelimwacha mtu kuongoza karne bora, lau kama kungelikuwa mwingine ambaye ni bora zaidi na mwenye kustahiki zaidi ukhaliyfah.
Tunaamini pia kuwa mmoja katika watu hawa anaweza kuwa na sifa ya kipekee yenye kumfanya akawa ni bora kuliko yule ambaye ni mbora zaidi kuliko yeye kwa jumla. Lakini hata hivyo haina maana ya kwamba anastahiki fadhila za moja kwa moja juu ya yule mwenye kumshinda, kwa sababu kuna mambo mengi mbali mbali yanayopelekea katika fadhila.
Tunaamini kuwa Ummah huu ndio Ummah bora na mtukufu zaidi kwa Allaah (´Azza wa Jall). Amesema (Ta´ala):

"Mmekuwa Ummah bora kabisa uliotolewa kwa watu: mnaamrisha mema na mnakataza munkari na mnamwamini Allaah." (03:110)
Tunaamini kuwa wabora wa Ummah huu ni Maswahabah, kisha Taabi´uun na halafu waliokuja baada yao.
Tunaamini kuwa kutakuwepo siku zote kikundi katika Ummah huu kilicho juu ya haki wazi wazi. Hakidhuriki na wale wenye kuwapinga na wenye kwenda kinyume nao mpaka ije amri ya Allaah (´Azza wa Jall).
Tunaitakidi kuwa matatizo yaliyotokea kati ya Maswahabah ilikuwa ni kwa sababu ya mitazamo waliokuwa wakionelea kuwa ni ya sawa. Aliyepatia anapata thawabu mara mbili na mwenye kukosea anapata thawabu mara moja na kosa ni lenye kusamehewa.
Tunaona kuwa ni wajibu kunyamazia makosa yao. Hivyo hatuwataji isipokuwa tu kwa njia na sifa nzuri wanazostahiki. Tunaisafisha mioyo yetu kutokana na vifundo na chuki kwao. Amesema (Ta´ala):
“Hawi sawa miongoni mwenu aliyetoa kabla ya Ushindi [wa Makkah] na akapigana. Hao watapata daraja kubwa kabisa kuliko wale waliotoa baada [ya ushindi] na wakapigana - na wote Allaah Amewaahidi Pepo.” (57:10)
Kadhalika amesema (Ta´ala) juu yetu:
“Na wale waliokuja baada yao [ ni wenye] kusema: “Mola wetu! Tusamehe na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa iymaan na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo kwa wale walioamini. Mola wetu! Hakika Wewe ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.” (59:10)